Thursday, December 2, 2010

SOKO KUU LA UHINDINI MBEYA LAWAKA MOTO

Takriban miaka mitatu baada ya kuungua kwa soko lililokuwa maarufu sana la Mwanjelwa, wakazi wa jiji la Mbeya, jana usiku wamekumbwa na simanzi kwa mara nyingine baada ya soko kuu la Uhindini, lililoko katikati ya jiji hilo kuteketea kwa moto.

Ingawa hadi sasa haijaweza kufahamika hasa nini chanzo cha moto huo wala hasara iliyotokana na moto huo, kumekuwa na taarifa zilizozagaa ambazo zinaelezea kuwa, chanzo cha moto huo ni hitilafu za umeme, ambao katika siku na muda wa tukio, ulikuwa unawaka na kukatwa kwa style ya indicator za gari.

Tukio la kuungua kwa soko hili, limeshabihiana sana na lile la miaka mitatu iliyopita wakati soko la Mwanjelwa lilipoungua, kwani ilikuwa kipindi kama hili, na hali hii imezua hofu miongoni mwa wakazi wa jijini hapa.

Mungu epushia mbali mabalaa haya. napenda kuwapa pole wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameathiriwa na tukio hilo, nikitaraji kuwa mamlaka husika zitafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kutupatia taarifa za kitaalamu, zitakazowezesha wananchi na wadau mbalimbali kuwa katika hali ya tahadhari ili majanga mengine ya namna hii yasiendelee kuukumba mji wa Mbeya na maeneo mengine ya nchi.

No comments:

Post a Comment