Thursday, December 2, 2010

PEPE KALEE MIAKA 12 SASA TANGU AFARIKI

Pepe Kalle Miaka 12 sasa Afrika bado yamlilia

Mbali na kuwa na utajiri wa madini ya kila aina, Bara la Afrika limejaaliwa kuwa na utitiri wa watu wenye vipaji katika nyanja mbalimbali katika ulimwengu huu.

Leo hii ukizungumzia mchezo wa soka basi ndani yake kutakuwa na mlolongo wa majina ya wasakata kabumbu, wanariadha, wanamuziki nakadhalika kutoka bara hili ambao wanatamba kote duniani.

Kwa namna moja ama nyingine hawa ni watu ambao tunaweza kuwaita mashujaa wa bara letu kwa kuweza kulitangaza vizuri kupitia fani zao mbalimbali.

Jumapili iliyopita Afrika ilikua inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 12 tangu kifo cha nyota wa muziki wa Kwasakwasa wa DRC Kongo, marehemu Kabesele Yampanya ‘Pepe Kalle’

Akiwa na sauti za mirindimo mbalimbali na uwezo wa kubadili mbinu zake za uchezaji wa shoo, Pepe Kale alirekodi nyimbo zaidi ya 300 na albamu zaidi ya 20 katika kipindi cha miongo miwili ya uimbaji wake.

Akijulikana kama Tembo wa Muziki wa Afrika, Pepe Kalle aliwafurahisha mashabiki wake kwa kiwango cha hali ya juu katika uimbaji na pia ubunifu wa mitindo kadhaa iliyokuwa ikinogesha muziki wake.

Alianza kuimba akiwa na bendi moja iliyojulikana kama African Jazz. Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mwalimu wake wa muziki, Grand Kalle. Baadaye alikuja kuwa mwimbaji mkubwa wa Bendi ya Lipua Lipua ambapo alikuwa akiimba sambamba na mwimbaji mwingine aliyejulikana kama Nyboma MwandidoMwaka 1972, akiwa na wanamuziki wengine, Dilu Dilumona na Papy Tex, waliiacha Lipua Lipua na kuunda bendi yao iliyojulikana kama Empire Bakuba. Bendi hiyo ilianza kwa kupiga muziki wake maeneo ya Jiji la Kinshasa.

Pepe Kalle akiwa na mwanamuziki mwingine Zaiko Langa Langa waliiwezesha bendi hiyo kuwa maarufu kwa vijana katika jiji la Kinshasa. Wakiwa na nyimbo kama Dadou alioutunga yeye mwenyewe na Sango ya Mawa uliotungwa na Papy Sango, bendi hiyo ilikuwa ikikamata nafasi za juu kabisa kwenye chati mbalimbali za muziki nchini Kongo. Pepe Kalle na Papy Sango pia ndiyo waliotunga staili ya kucheza iitwayo Kwasakwasa.

Katika maadhimisho yao ya miaka 10 mwaka 1982, bendi yao hiyo ilipigiwa kura kuwa bendi bora zaidi nchini Zaire (sasa DRC Kongo). Katika miaka ya 1980, Empire Bakuba iliendelea kufanya shoo katika maeneo mengi huku ikitoa si chini ya albamu nne kwa mwaka.

Mwaka 1986, Pepe Kale akishirikiana na Nyboma, alitoa albamu iitwayo Zouke Zouke ambayo ilikuwa ni moja ya albamu zilizouza vizuri kwa miaka mingi. Lakini ushirikiano wa mwaka 1988 na Nyboma katika albamu iliyoitwa Moyibi ndiyo uliompa heshima kubwa katika Bara la Afrika.

Mwaka 1990, Pepe Kalle alitoa albamu ijulikanyo kwa jina la Roger Milla. Albamu hiyo aliitoa kwa heshima ya mwanasoka wa Cameroon aliyetesa enzi hizo, Roger Milla.

Mwaka 1992, bendi yake ya Empire Bakuba ilipata pigo kubwa la kwanza baada ya kifo cha mcheza shoo, Emoro aliyekuwa mfupi aliyeuawa walipokuwa nchini Botswana walikokwenda kufanya shoo.

Pamoja na pigo hilo, umaarufu wa Pepe Kalle uliendelea kuongezeka katika miaka ya 1990 ambapo alitoa albamu kama Gigantafrique, ‘Larger than life’ na ‘Cocktail’ zilizopendwa na mashabiki wengi.

Pepe Kalle alizaliwa Novemba 30, 1951 Jina lake halisi ni Kabasele Yampanya, alikufa Novemba 28, 1998 kwa shinikizo la damu.

No comments:

Post a Comment